Friday, March 27, 2015

USHIRIKIANO! KAGAME AMWAGIA SIFA KIKWETE.






Rais wa Tanzania mh Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa kenya mh Paul kagame wakiteta jambo wakati wa mkutano uliwakutanisha wakuu wa nchi wa ukanda wa kati, Dar es salaam Tanzania.

Dar es Salaam. Rais wa Rwanda, Paul Kagame amemwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa kuboresha huduma za Bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda kufika mapema zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Akizungumza kwa furaha wakati marais hao walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio kwa Rwanda.
Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu Rwanda tunafaidika,” alisema Rais Kagame. Alisema Rwanda itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ili kuhakikisha kuwa wananchi wote wananufaika kibiashara.
Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani, ameitembelea Bandari ya Dar es Salaam mara nne, lakini ziara tatu za mwanzo hazikuwa za furaha kutokana na wizi, ucheleweshaji wa mizigo na malalamiko yaliyokuwa yamekithiri bandarini hapo.
Huku akionekana mwenye furaha, Rais Kikwete alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatakiwa ipongezwe kwa kufanikiwa kuwaondoa wezi waliokuwa wakiirudisha nyuma.
“Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kutokana na uhalifu uliokuwa unafanyika bandarini hapo, Burundi nayo ilikuwa ikiilalamikia Tanzania.
“Burundi walilalamika mambo tunayowafanyia, lakini ukiwaangalia ni kama vile wanamlaumu Mungu kwa nini aliiweka Tanzania katikati yao na bahari, pengine ingekuwa nchi nyingine ingewafanyia tofauti,” alisema Rais Kikwete.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadhi Massawe alisema tangu kufanyika kwa maboresho bandarini hapo, idadi ya mizigo inayopelekwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda imeongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TICTS, Walles Paul alisema pamoja na kitengo hicho kuboresha utoaji wa huduma zake, bado kinakabiliwa na changamoto ya eneo la kufanyia kazi.
“Nafasi haitoshi tunahitaji kuongezewa ili tusirudi nyuma tulikotoka,” alisema Paul.
Mapema jana asubuhi katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa wawekezaji, Rais Kagame alisema ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya uchukuzi hasa reli inaboreshwa.

No comments:

Post a Comment