Wednesday, March 11, 2015

NIYONZIMA AGOMA KUSAINI MKATABA MPYA YANGA

YANGA wajanja sana, kwani wanataka Haruna Niyonzima asaini mkataba mpya na klabu yao halafu malipo yafanyike baadaye kwa awamu jambo ambalo limepingwa na kiungo huyo raia wa Rwanda.
Niyonzima ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga ambao mikataba yao itafikia tamati mwishoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara ifikapo Mei, mwaka huu.Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa kiungo huyo, jamaa huyo amesitisha mazungumzo yoyote kuhusu usajili na Yanga kwani uongozi haukumuonyesha dalili za kumpatia fedha badala ya kumtaka asaini kwanza halafu malipo baadaye.
“Wamemuambia asaini kwanza halafu malipo baadaye, hilo jambo limemuudhi na ameona kama anadharauliwa kwani kwa thamani yake si mtu wa kusaini kwa mali kauli, hivyo sasa anajipanga kutafuta timu nyingine,” alisema rafiki huyo.
Mwandishi wetu alipomtafuta Niyonzima alisema: “Siwezi kusema lolote rafiki yangu kwani ninachojua nimebakiza miezi michache kabla ya mkataba wangu kuisha, baada ya hapo nitakuwa na jibu la kukupa, kwa sasa wacha niitumikie Yanga.”
Hata hivyo, blogu hii inafahamu kuwa Niyonzima yupo katika harakati za kusaka timu mpya kwani haoni dalili za kupewa usajili mpya wa donge nono kwenye kikosi hicho.“Mimi kazi yangu ni mpira, hivyo timu yenye fedha ikinifuata kuzungumza nami nitaisikiliza kuhusu ofa yao japokuwa naipa kipaumbele Yanga kwanza,” alisema Niyonzima.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga, Seif Ahmed ‘Seif Magari’, alisema: “Hilo suala muulize mwenyekiti Chanji (Isaac), maana ndiye anajua jinsi ya kukujibu.”
Chanji hakuweza kupatikana kwani simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa na hata Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, hakuweza kupatikana.
Baadhi ya wachezaji wengine wa Yanga wanaomaliza mikataba yao baada ya ligi kuisha ni Mrisho Ngassa, Said Bahanuzi anayecheza kwa mkopo Polisi Moro na Mbuyu Twite.
by TEGE INC BLOG.

No comments:

Post a Comment