Rais wa Tanzania mh Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa kenya mh Paul kagame wakiteta jambo wakati wa mkutano uliwakutanisha wakuu wa nchi wa ukanda wa kati, Dar es salaam Tanzania.
Dar es Salaam. Rais wa Rwanda, Paul Kagame
amemwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa kuboresha huduma za Bandari ya
Dar es Salaam na kuwezesha mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda kufika
mapema zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Akizungumza kwa furaha wakati marais hao
walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS
bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio
kwa Rwanda.
“Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio
yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu
Rwanda tunafaidika,” alisema Rais Kagame. Alisema Rwanda itaendeleza
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ili kuhakikisha kuwa
wananchi wote wananufaika kibiashara.
Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani,
ameitembelea Bandari ya Dar es Salaam mara nne, lakini ziara tatu za
mwanzo hazikuwa za furaha kutokana na wizi, ucheleweshaji wa mizigo na
malalamiko yaliyokuwa yamekithiri bandarini hapo.
Huku akionekana mwenye furaha, Rais Kikwete
alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatakiwa ipongezwe kwa
kufanikiwa kuwaondoa wezi waliokuwa wakiirudisha nyuma.
“Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa
mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa
siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna
udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kutokana na uhalifu uliokuwa unafanyika bandarini hapo, Burundi nayo ilikuwa ikiilalamikia Tanzania.
“Burundi walilalamika mambo tunayowafanyia, lakini
ukiwaangalia ni kama vile wanamlaumu Mungu kwa nini aliiweka Tanzania
katikati yao na bahari, pengine ingekuwa nchi nyingine ingewafanyia
tofauti,” alisema Rais Kikwete.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadhi Massawe
alisema tangu kufanyika kwa maboresho bandarini hapo, idadi ya mizigo
inayopelekwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda
imeongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TICTS, Walles Paul alisema
pamoja na kitengo hicho kuboresha utoaji wa huduma zake, bado
kinakabiliwa na changamoto ya eneo la kufanyia kazi.
“Nafasi haitoshi tunahitaji kuongezewa ili tusirudi nyuma tulikotoka,” alisema Paul.
Mapema jana asubuhi katika hotuba yake ya ufunguzi
wa mkutano wa wawekezaji, Rais Kagame alisema ili kuendana na kasi ya
ukuaji wa uchumi, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya uchukuzi hasa
reli inaboreshwa.